Job 21

Hotuba Ya Saba Ya Ayubu

Ayubu Anajibu: Waovu Mara Nyingi Huenda Bila Kuadhibiwa

1Ndipo Ayubu akajibu:
2 a“Yasikilizeni maneno yangu kwa makini;
hii na iwe faraja mnayonipa mimi.

3 bNivumilieni ninapozungumza,
nami nikishazungumza, endeleeni kunidhihaki.


4 c“Je, kwani malalamiko yangu yanaelekezwa kwa mwanadamu?
Kwa nini nisikose subira?

5 dNiangalieni mkastaajabu;
mkaweke mkono juu ya vinywa vyenu.

6 eNinapowaza juu ya hili, ninaogopa,
nao mwili wangu unatetemeka.

7 fKwa nini waovu wanaendelea kuishi,
wakifikia umri wa uzee na kuendelea kuwa na nguvu?

8 gHuwaona watoto wao wakithibitika
wakiwa wamewazunguka,
wazao wao mbele za macho yao.

9 hNyumba zao zi salama wala hakuna hofu;
fimbo ya Mungu haiko juu yao.

10 iMadume yao ya ng’ombe huvyaza bila kushindwa kamwe;
ng’ombe wao huzaa wala hawaharibu mimba.

11 jHuwatoa watoto wao nje kama kundi;
wadogo wao huchezacheza.

12 kHuimba nyimbo kwa matari na kwa kinubi,
nao huifurahia sauti ya filimbi.

13 lHuitumia miaka yao katika mafanikio
nao hushuka kaburini kwa amani.

14 mLakini humwambia Mungu, ‘Tuache sisi!’
Hatuna haja ya kufahamu njia zako.

15 nMwenyezi ni nani hata tumtumikie?
Tutapata faida gani kumwomba?

16 oLakini kufanikiwa kwao hakupo mikononi mwao wenyewe,
hivyo najitenga mbali na shauri la waovu.


17 p“Lakini ni mara ngapi taa ya waovu huzimwa?
Ni mara ngapi maafa huwajia,
yale yawapatayo ambayo Mungu
huwapangia katika hasira yake?

18 qNi mara ngapi huwa kama majani makavu mbele ya upepo,
kama makapi yachukuliwayo na dhoruba?

19 rImesemekana, ‘Mungu huiweka akiba adhabu ya mtu
kwa ajili ya wanawe.’
Mungu na amlipe mtu mwenyewe,
ili apate kulijua!

20 sMacho yake mwenyewe na yaone maangamizi yake;
yeye na ainywe ghadhabu ya Mwenyezi.

21 tKwani anajali nini kuhusu jamaa anayoiacha nyuma,
miezi yake aliyopangiwa ifikapo mwisho?


22 u“Je, yuko mtu yeyote awezaye kumfundisha Mungu maarifa,
iwapo yeye ndiye ahukumuye hata walio juu ya wote?

23 vMtu mmoja hufa akiwa na nguvu zake kamili,
akiwa salama na mwenye raha kamili,

24 wmwili wake ukiwa umenawiri,
nayo mifupa yake ikiwa imejaa mafuta ndani yake.

25 xMtu mwingine hufa katika uchungu wa nafsi,
akiwa hajafurahia kamwe jambo lolote zuri.

26 yHao wote hulala mavumbini,
nao mabuu huwafunika wote.


27 “Ninayajua kikamilifu yale mnayoyafikiri,
mipango ambayo kwayo mngenitendea mabaya.

28 zMwasema, ‘Iko wapi sasa nyumba ya huyo mtu mkuu,
mahema ambayo watu waovu walikaa?’

29 Je, hamkuwahi kuwauliza hao wanaosafiri?
Je, hamkutafakari taarifa zao:

30 aakwamba mtu mwovu huepushwa kutoka siku ya maafa,
kwamba huokolewa kutoka siku ya ghadhabu?

31 abNi nani hulaumu matendo yake mbele ya uso wake?
Ni nani ampatilizaye kwa yale aliyoyatenda?

32 acHupelekwa kaburini,
nao ulinzi ukawekwa kwenye kaburi lake.

33 adUdongo ulio bondeni ni mtamu kwake;
watu wote watamfuata,
nao umati wa watu usiohesabika umemtangulia.


34 “Hivyo ninyi mnawezaje kunifariji kwa upuzi wenu?
Hakuna kilichosalia cha majibu yenu isipokuwa uongo!”
Copyright information for SwhKC